Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya Kanda ya Kati Dodoma imekabidhi silaha mbili za moto kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya zilizokamatwa kwenye operesheni zilizofanyika April 24 hadi 28,2024 mkoani humo.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, hii leo Mei 3, 2024 katika ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Kaimu Kamishna Msaidizi Kanda ya kati, Mzee Kasuwi amesema, silaha hizo aina ya gobore zilikuwa zinamilikiwa na Hamisi Chambo (46) na Abdilah Juma (45) wote wakazi wa kata ya Segera na zilikuwa zikitumika kulinda mashamba ya bangi.

Aidha, Kamishna Kasuwi amewaomba Wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa kupiga simu bure kupitia namba 119.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (RPC) Theopista Mallya ameishukuru Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kutokomeza uhalifu na kutoa rai kwa wananchi kufuata sheria za nchi na taratibu zake kwani Jeshi la polisi lipo na litaendelea kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya.

Silaha zilizokabidhiwa, zilikamatwa katika operesheni iliyofanyika maeneo ya wilaya ya Chamwino na Dodoma mjini ambapo jumla ya ekari 9.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa, kilogramu 156.23 za bangi na misokoto 127 ya bangi zilikamatwa ambapo watuhumiwa 16 wanashikiliwa kuhusika na dawa hizo.

Majaliwa: Watendaji ondoeni ukiritimba utoaji wa Habari
CHADEMA kwafukuta: Lissu adai rushwa imekithiri ndani ya chama