Uongozi wa Simba SC wamemwambia wakala wa mastaa wawili Bakari Nondo Mwamnyeto na Kibu Denis achague moja au akose yote.
Ambakishe Kibu pale Simba SC ili wamnunue Nondo kwa pesa nzuri au amuachie Kibu aende Young Africans na wao Simba wamnunue Nondo kwa pesa ya chini, halia mbayo inadaiwa kumpa wakati mgumu wakala huyo wa wachezaji hao, Carlos Slyvester.
Taarifa zinaeleza kuwa mabosi wa Simba SC wanatarajiwa kuwa na kikao leo Alhamis (Mei 09) na wakala wa wachezaji hao baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC kwa ajili ya kujadili dili la Mwamnyeto kutua Msimbazi lakini pia kwa sharti la kumbakisha Kibu anayewinda na watani zao Young Africans.
Hivi karibuni imefahamika kuwa Kibu yupo kwenye rada za kuwindwa na Young Africans na mambo yakienda vizuri atasaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo msimu ujao lakini Simba SC wanakomaa abaki ingawa presha zimekuwa nyingi kutoka ndani na nje ya klabu.
Viongozi wanadai kwamba kuna presha za makusudi za kuwatumia mpaka watu wa ndani ya klabu kutaka mkwanja na thamani ya Kibu iongezwe kiaina.
Picha limeanza upya baada ya Simba SC kuonyesha kutokubaliana na Kibu kwenda Young Africans, hivyo imempa mtihani mzito wakala wa wachezaji hao kuhakikisha wote wawili wanacheza Msimbazi msimu ujao, ingawa Young Africans nao wanaona kama kuna udalali wa kisirisiri kutaka kuipandisha thamani na dau la usajili mpya wa Mwamnyeto ingawa wanajipa kokote.
Simba SC wanapambana kuhakikisha Kibu anasalia klabuni hapo, licha ya kwamba hana namba za kuvutia uwanjani, kwani kwa mastraika wazawa bado anaonekana lulu na wakimuuzia adui ni hatari kubwa.
Alipotafutwa wakala huyo, amesema ni kweli amepokea ofa kutoka Simba SC na Young Africans, wanaendelea kuzifanyia kazi, timu ambayo itafikia maslahi basi itafanikisha saini ya mteja wake ingawa lolote linaweza kutokea.
“Kwa pande zote mbili Simba SC na Young Africans mazungumzo yapo na yanaendelea vizuri, pia sio ofa hizo tu, zipo nyingine kutoka nje ya Tanzania lakini hatuwezi kuweka wazi kwa sasa,” amesema na kuongeza;
“Kwa timu zote mbili bado makubaliano hayajafikiwa mambo yakienda sawa moja kati ya timu hizo kila kitu kitawekwa wazi mtafahamu kwani mchezo wanaocheza wachezaji ni wa wazi,” amesema Carlos.
Kibu ambaye msimu huu anamiliki bao moja kwenye mechi za Ligi Kuu ni kati ya wachezaji wanaoonekana wana bei kubwa sokoni, akielekea kumaliza mkataba mwishoni mwa 2023/24.
Kati ya timu zilizoingia vitani kuhitaji saini yake ni Young Africans inayotajwa kupeleka ofa ya Sh300 milioni, Ihefu FC yenyewe katika ofa yake iko tayari kutoa kiasi cha Sh500 milioni kwa mkataba wa miaka mitatu lakini kwa awamu, huku waajiri wake wakiweka mezani Sh 300 lakini wakitoa kwa awamu.
Wakati Simba wakitoa sharti hilo kwa wakala wa Mwamnyeto, yeye Kibu anaonekana hataki kusalia kabisa kikosini, sababu zikitajwa kuchukizwa na kuchukuliwa kama mchezaji wa kawaida wakati amekuwa akipambana kwa ajili ya timu.
Imeelezwa beki Mwamnyeto naye hataki kusalia Young Africans, baada ya kuona uongozi wa timu hiyo hautaki kumpa thamani yake wakati ameisaidia timu hiyo kunyakua mataji mawili ya Ligi Kuu akiwa nahodha.
Jina la Mwamnyeto kuhusishwa na Simba SC sio kitu kigeni Agosti Mosi, 2020 Young Africans iliwapiga bao watani wao kwa kumsaini mchezaji huyo kwa mkataba wa miaka miwili.
Hivyo hivyo kwa upande wa Kibu kwa mara ya kwanza anajiunga Simba SC msimu wa 2021/22 na akaifungia timu hiyo mabao manane na kutoa pasi tatu zilizozaa mabao.