Ila Wanaume! ama kweli Wanaume ni hatari kwa afya’ yaani kuna matukio huwa wanafanya kiasi ukisimuliwa unashangaa unajihisi kwenye hii dunia wewe ni mgeni umetokea Sayari ya jirani. Inastaajabisha na inafikirisha nadhani hata shetani kuna muda huwa anashangaa, “Wanaume wamepigaje hapo”.

Hebu fikiria mdada wa watu anaamka asbhi halafu unagundua kuwa mumewe wa kitambo, aliyemlelea mtoto na wamekuwa wakiishi maisha mazuri miaka yote si mume wake halali kwa zaidi ya miaka 20 nyuma licha ya kuwa ameamka naye siku hiyo na walifunga ndoa Kanisani.

Hili ndilo lililomtokea mwanamama Cristina Carta Villa, mke wa ‘mwamba’ Gabriel Villa ambaye aligundua kwamba mumewe alimtaliki kwa siri miezi michache tu baada ya harusi yao miaka 20 nyuma, akidai alifanya hivyo ili kulinda mali zake akihofia kufanyiwa ‘umafia’ na mkewe.

Gabriel Villa (kushoto), na mkewe Cristina Carta.

Jinsi walivyokutana.

Mwaka 1994, Gabriel Villa alikutana na Christina Carta kwenye karamu na walifurahiana sana kisha kukurubiana kwamba wawe wapenzi, hali iliyopelekea kufuata taratibu na wakaoana, ingawa Christina alikuwa ni mdogo kwa Gabriel akizidiwa kwa miaka 31.

Maisha yao ya ndoa yalikuwa yenye furaha kwa miaka 20 kwa jinsi anavyosimulia Christina, maana wakati wote alipokea huba zito la mumewe na alijua kwamba mambo ni shwari hakuna hatari wala mashairi.

Maisha yao.

Christina anasema, licha ya tofauti yake ya umri na Gabriel (yeye 59 na mumewe 90), waliishi kwa upendo na hata walipo oana walitumia miongo miwili kufurahia maisha na kutengeneza safari kadhaa za kwenda kuhuisha ndoa yao ikiwemo kuwekeza vitega uchumi huko Manhattan, Ufaransa na Massachusetts.

Walipata mtoto wa kiume, aliyemlea akiwa mgonjwa, akisema licha ya changamoto hiyo bado alikuwa mke na mama mwenye upendo na kujali na hata siku moja hakuwahi kuona dosari katika kuishi kwake na mumewe, yaani kila kitu kilikuwa sawa.

Chanzo cha tatizo.

Christina anasema siku moja akiwa katika harakati za kupanga makabrasha aliona bili ya kodi ya nyumba yao ya Manhattan iliyofika kwa barua ikiwa na jina la Gabriel pekee na lake halimo, akashtuka.

Alipochunguza kwa makini, aligundua kwamba kuna baadhi ya mambo hayapo sawa na ni ya muda mrefu, ikiwemo kuuzwa kwa baadhi ya mali za familia yake bila kuhusishwa kitu ambacho kilimsikitisha na hata alipohitaji maelezo ya mumewe, hayakujitosheleza.

Christina hatimaye baada ya kufikiri kwa kina aliamua kwamba aende kwenye vyombo vya sheria kudai talaka, lakini alipofika kwa wakili wake, alishtuka kusikia kwamba tayari alikuwa ameachana na Gabriel miaka 20 iliyopita.

Talaka ya siri.

Ilibainika kuwa bila kujua au ridhaa yake, Gabriel alikuwa amemtaliki miezi minne tu baada ya harusi yao na hata ile bili ya nyumba ya Manhattan aliyoiona, ilitokana na Gabriel kutumia karatasi za talaka kujaribu kuondoa jina la Cristina kwenye hati ya ghorofa, ambayo Cristina anaamini kwamba Gabriel alitaka kuuza.

Kwanini alipewa talaka ya siri.

Baada ya kufunga ndoa, miezi minne mbele wanandoa hao walienda Jamhuri ya Dominika kwa mapumziko, na wakiwa huko Gabriel alimtaliki kwa makusudi, sababu nchi hiyo ndiyo ya pekee ambayo mtu mmoja anaweza kuwasilisha talaka, bila kumjulisha mwenzake.

Gabriel anasema alifanya hivyo kwa sababu alijua siku moja Christina angemtaliki na kujaribu kuchukua pesa zake, hivyo aliona njia sahihi na pekee ya ulinzi ‘shirikishi’ wa mali zake ni kuratibu safari kwenda taifa hilo la Dominika, ili kuweka ‘anti-virus’ (daah nacheka kama mazuri),…. Gabriel amenishinda tabia.

Christina anasema, “talaka hiyo ni ulaghai, na nilimshtaki Gabriel kubatilisha ile talaka na kumzuia asigawe nyumba yetu. Sasa ninatambua kwamba katika miaka hii yote ya shangwe na furaha, na nyakati ngumu tulizoshiriki pamoja, mume wangu alinidanganya na alikuwa na talaka ya Wadominika nyuma ya akili yake, niliumia.”

Kuhusu utaratibu.

Vipi mwenzangu, we unaweza kumtaliki mtu kimya kimya na ukawa unaishi naye? maana Cristina anasema talaka ilikuwa ya ‘mchongo’  kwa sababu yeye hakuwa na jinsi na wala hakuwa anaifahamu na mbaya zaidi hakuna gazeti lililoweka notisi ya talaka, kama inavyotakiwa na sheria ya Dominika.

Kiukweli yupo sahihi, kwani kiutaratibu hata pale Washington hakuna Mahakama ambayo ingekubali talaka ya bandia kama hiyo, haikuwa ya kimaadili na ni kinyume cha sheria. Hapa kwetu hapa tunaiita ni batili, lakini ilikuwaje ‘mwamba’ akafanikisha hiyo talaka? ndilo swali ambalo linamsumbua Christina.

Kikao cha Wanaume.

Lazima kifanyike, ni cha kujadili tu hili tukio sema kitafanyika siku zijazo, mahali na muda tutajuzana, yaani ni lazima tupate ukweli na kujua kisa hasa cha Gabriel kutuwakilisha kwa taswira hasi namna hii, ambayo imeacha alama mbaya katika maisha kwa shemeji yetu Cristina.

Udhibiti wahamiaji haramu: Ulinzi kuimarishwa mpakani
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Mei 12, 2024