Vinara wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara Young Africans leo Jumatatu (Mei 13) watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
Ni mechi muhimu kwa timu zote mbili kwani ushindi kwa Young Africans kwenye mchezo wa leo Jumatatu (Mei 13) kutawafanya kuhitaji alama mbili katika mechi zao tatu zilizobaki kutetea ubingwa wao.
Kwa sasa Young Africans inayonolewa na Kocha Miguel Gamondi kutoka Argentina inahitaji alama nne kwenye mechi zao nne zilizosalia kunyakua ubingwa huo.
Huku Mtibwa wakipambana kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja baada ya kutoka kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United Uwanja wa Manungu na kufikisha alama 20 katika mechi 26 walizocheza.
Kama itapoteza mchezo wa leo Mtibwa itaendelea kubaki mkiani na kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu walipopanda mwishoni mwa miaka ya 1990.
Mechi nyingine za Ligi hiyo Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Ihefu Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Dodoma Jiji kwenye mchezo uliopita, Prisons watahitaji kupata alama tatu dhidi ya Ihefu kuwa kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kushika nafasi ya nne na kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika (CAF) mwakani.
Prisons wana alama 33 kwenye mechi 26 walizocheza mpaka sasa, huku Ihefu wakihitaji alama tatu baada ya kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya JKT Tanzania kwenye mchezo uliopita.
Mechi nyingine JKT Tanzania watakuwa wenyeji wa Singida Fountain Gate Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es salaam.