Wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea kutekeleza mradi wa mnara wa mtandao ulipo Wilayani Manyoni Mashariki katika kata ya Iseke iliyopo kijiji cha Igwamadete Mkoani Singida.
Akizungumza na Wananchi katika kijiji hicho mara baada ya kukagua mradi Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi ambapo amesema mradi huo umebakiza siku mbili ili kukamikika kwake.
“Leo tumekuja kukagua mnara unavyotekelezwa na furaha yangu kubwa ni kuwa zimebaki wiki mbili ili mradi huu ukamilike na sisi tuanze kupangusa simu zetu popote pale ambapo tutakuwepo, hii ni furaha kubwa sana kwetu,” amesema.
Mahundi amesema, “tuna minara kumi na tano (15) tunaenda kuijenga kwenye kata zetu hizi na katika minara yote tunayoenda kuijenga huu ndio mnara mkubwa kuliko minara yote ambayo itaenda kusimama.”
“Na kupitia ukubwa wa mnara huu tunajua mnaenda kupata mawasiliano mazuri, na katika kujiandikisha kwenye anuani za makazi,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF), Pius Joseph kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa mfuko huo amesema kutokana na urefu na jinsi ulivyojengwa kitaalamu mnara huo utawezesha makampuni mengine kuweza kuweka mitambo yao.
“Kampuni nyingine wanauwezo wa kuweka mitambo yao na kutoa huduma nyingine siyo Airtel peke yake kwamaana ya radio station na mitambo mengine”,amesema
Hata hivyo amesema mnara huo ni moja kati ya minara 758 ambayo imepangwa kujengwa.