Zanzibar na Comoro ni nchi ambazo zina Mahusiano maalum ya kuchanganya damu wa kindugu hali iliyopelekea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuridhia kufunguliwa kwa Konseli Mkuu wa Comoro Zanzibar.
Hayo yamebainika hii leo Mei 14, 2024 kupitia Rais Mwinyi wakati alipokutana na Balozi mpya wa Tanzania katika visiwa vya Comoro Saidi Yakubu, aliyefika kumuaga baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Mwinyi pia amemtaka Balozi Yakubu kuangalia fursa zilizopo za kuuza bidhaa mbalimbali kutoka nchini na kuzisimamia hati za makubaliano ya pamoja na kamati ya ushirikiano wa kudumu ikiwemo katika sekta ya afya, elimu, utamaduni, biashara, usafirishaji na habari.
Amesema Shirika la Meli la Zanzibar lina mpango wa kuagiza meli mbili mpya, ameleeza pia MV.Mapinduzi imeshafanyiwa ukarabati na hivi karibuni itaanza safari zake kutoka Zanzibar kwenda Comoro, ambapo pia wamejipanga kwa utalii wa matibabu kwa kuifanya Hospitali mpya ya Lumumba kuwa kituo cha kupokea wagonjwa kutoka nje hasa nchi ya Comoro pindi itakapokamilika na kuanza kutoa huduma.
Naye Balozi Yakubu amemuahidi Rais Dk.Mwinyi kudumisha uhusiano wa kindugu uliopo kati ya Zanzibar na Comoro pamoja na kuendeleza hati za makubaliano ya pamoja na Kamati ya ushirikiano ya kudumu.