Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wapo katika hatua nzuri kumsajili Mlinda Lango wa Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya, katika dirisha kubwa litakalofunguliwa baada ya kumalizika msimu huu 2023/24.

Young Africans inahitaji saini ya Mlinda Lango huyo ili kuwaongezea nguvu na ushindani makipa Djigui Diarra na Abutwalib Mshery katika kikosi chake msimu ujao 2024/25.

Kakolanya aliyewahi kukipiga katika kikosi cha Young Africans kuanzia mwaka 2016 hadi 2019, atakuwa mchezaji huru mwishoni mwa msimu huu baada ya kumaliza mkataba wake katika kikosi cha Singida Fountain Gate.

Kwa mujibu wa wa taarifa za uhakika zinaeleza kuwa Young Africans imeshafanya mazungumzo ya awali na Mlinda Lango huyo wa zamani wa Simba SC na yamefikia katika hatua nzuri.

“Mchezaji (Kakolanya) yupo tayari kurudi Young Africans, lakini wanasubiri mkataba wake umalizike na Singida Fountain Gate ndiyo apewe mkataba,” zimeeleza taarifa hizo

Taarifa hizo zimeongeza kuwa uongozi wa Young Africans umekuwa na mpango wa kumrejesha Kakolanya baada ya kocha wa kikosi hicho, Miguel Gamondi, kutaka Mlinda Lango mzawa mwenye uzoefu wa kutosha katika Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuimarisha kikosi chake.

“Majina ya Kakolanya na Mlinda Lango wa Tanzania Prisons, Amosi Yona, ndiyo yalikuwa yanajadiliwa, lakini viongozi wakakubaliana wamchukue Kakolanya, kufuatia kuwa mbioni kuachana na kipa Metacha Mnata.”

Hata hivyo Afisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amesema hivi sasa nguvu zao wamezielekeza katika mnichezo iliyosalia ya Ligi Kuu na nusu fainali ya Kombe la FA.

“Tukimaliza michezo yote kila kitu kitakuwa hadharani, nani anabaki na (nani) kuondoka tutajua wakati ukifika, kwa sasa mashabiki wetu waendelee kutupa sapoti. Pamoja na kuwa tayari tumekuwa bingwa, tunataka kushinda michezo iliyosalia.”

Kakolanya ambaye amesimamishwa na uongozi wa klabu ya Singida kwa madai ya kuondoka kambini bila ruhusa, amecheza mechi 10 na kuruhusu mabao 14, katika Ligi Kuu msimu huu na kuweka rekodi.

MAISHA: Asili ya Chui katika mila za Congo
Frimpong aweka masharti kubaki Leverkusen