Ili kuokoa maisha ya Watu na Mazingira, ajenda ya kutumia Nishati Safi ya kupikia ni ya muhimu ambapo tayari Serikali inashirikisha sekta binafsi ikilenga kuhakikisha uwezo wa Wananchi katika kumudu, upatikanaji na kujenga uelewa kwa Wananchi kutumia Nishati Safi badala ya kuni na mkaa.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo wakati wa mkutano wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus na Viongozi wengine na Vyombo vya Habari, Ikulu jijini Dar es Salaam hii leo Mei 17, 2024.

Amesema, Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia umefanikiwa kwa asilimia kubwa chini ya Kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wenyeviti wenza, ambao wamewezesha upatikanaji wa Dola za Kimarekani bilioni 2.2.

Dkt. Jafo pia amesema, Uingereza nayo imeahidi kutoa Dola za Kimarekani 3.4 milioni kwa Tanzania ikiwa ni mafanikio yaliyopatikana katika mkutano na ni fursa kwa nchi katika kuchagiza matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua itakayowasaidia akinamama na wasichana kuzalisha na kusoma badala ya kutafuta kuni.

Waziri Jafo amesema Tanzania imejipambanua katika ajenda ya nishati safi kwa kuwa na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao ni nyenzo muhimu ya kukabiliana na athari za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Mei 18, 2024
Ujio wa uchaguzi: TAKUKURU yautahadharisha umma