Kukata Tamaa ni Dhambi Kubwa ya Kufikia Mafanikio, ni kauli ambayo huenda ikawa inatumiwa sana katika Mazoezi na Chumba Cha kubadilishia cha Simba SC, katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu 2023/24.
Simba SC inawania nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuukosa Ubingwa ulioendelea kusalia kwa Watani zao wa Jadi (Young Africans), ambao wameendelea kuwa wafalme za Soka la Bongo.
Kwa kudhihirisha kauli hiyo ina nafasi kubwa Simba SC kwa sasa, Kaimu Kocha Mkuu wa kikosi hicho cha Msimbazi Juma Ramadhan Mgunda amesisitiza kuwa mapambano bado yanaendelea na kikosi chake kitapambana hadi dakika ya mwisho.
Akiwa katika Mkutano na Waandishi wa Habari mapema leo Jumatatu (Mei 20), Kocha huyo mzawa amesema pamoja na Bingwa wa Tanzania Bara kupatikana, bado kikosi chake kina lengo la kusaka nafasi ya kwenda kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu ujao 2024/25.
Mgunda ametoa kauli hiyo kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Geita Gold FC utakaopigwa kesho Jumanne (Mei 21), Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam.
“Unapohitaji kitu ni lazima uwe umejiandaa kukipata, kwa hiyo sisi Simba SC tunajua tunahitaji nini. Kwa hiyo tunafahamu kuwa ili kufikia malengo yetu tunapaswa kupambana na kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama tulivyojiandaa”
“Hii ni ligi na sisi ni washindani kwa hiyo sisi tumejiandaa kwenda kupambana na Geita Gold, haijalishi wapo kwenye nafasi gani, tunawaheshimu. Wanashindana na wana malengo yao na sisi tuna malengo yetu, hivyo sisi tumejiandaa kwenda kupambania alama tatu muhimu.”
“Tunacheza na Timu nzuri yenye kushindana na yenye malengo yake, kwa hiyo kwa kuwa sisi tupo kwenye mbio za kusaka nafasi ya pili, tutaingia Uwanjani tukiwapa heshima yao kama timu kwa sababu tunafahamu wana kocha mzuri na kikosi kizuri, kikubwa lengo letu ni kusaka alama tatu. Kipekee niseme kuwa huu ni mchezo muhimu kwa pande zote mbili.” amesema Mgunda
Simba SC kwa sasa imefikisha alama 60 sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na uwiyano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.