Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umewataka Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa mwishoni mwa juma hili.
Young Africans ilijihakikishia kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo, baada ya kuifumua Mtibwa Sugar mabao 3-1, juma lililopita katika uwanja wa Manungu Complex, mkoani Morogoro.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Ally Kamwe mapema leo Jumatatu (Mei 20) alizungumza na Waandishi wa Habari na kufichua kuwa, timu yao itakabidhiwa Kombe la Ubingwa baada ya mchezo wa dhidi ya Tabora United.
Kamwe amesema mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku akiwaahidi Mashabiki na Wanachama wao zawadi nono, ambayo itaambatana na Burudani kabla ya baada ya mchezo huo utakaopigwa Mei 25.
“Kwenye mechi ya kukabidhiwa Ubingwa dhidi ya Tabora tutakuwa na jambo kubwa na la kihistoria kwenye mechi za kukabidhiwa Ubingwa katika nchi hii. Mwananchi ukikosa hii surprise ya kipekee basi ujilaumu wewe mwenyewe. Popote ulipo anza safari uje kwenye Jumamosi ya Kibingwa.
“Siku ya kukabidhiwa Ubingwa tutakuwa na MaDJ watakaokuwepo. Kuanzia leo tutaanza kutaja orodha ya MaDJ watakaotupatia burudani ya Ubingwa akiwemo DJ Ally B. Tutataja na wasanii wakubwa ambao tutawashusha kwa Mkapa” amesema kamwe Ally Kamwe
Katika hatua nyingine Ally Kamwe amesema kikosi chao kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam kuelekea Dodoma mapema kesho Jumanne (Mei 21), tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma jiji utakaopigwa keshokutwa Jumatano (Mei 22).
“Kesho tunasafiri majira ya saa nne asubuhi kuelekea pale mkoani Dodoma kucheza dhidi ya Dodoma Jiji. Mchezo huo utafanyika tarehe 22 Mei 2024. Mechi hii ya Dodoma tumeifanya mechi ya kushukuru benchi la ufundi. Hivyo itakuwa ni Gamondi Day.
“Kwenye Gamondi Day itakapofika dakika ya 30, wana Yanga wote tunapaswa kusimama kumpigia makofi Gamondi na benchi lake la ufundi kwa dakika moja. Tunampa heshima Gamondi kwa kutupatia ubingwa wa kishitoria mara ya 30” amesema Ally Kamwe
Wakati huo huo Klabu ya Young Africans imealikwa Bungeni Jijini Dodoma na mwenyeji wao Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk. Damas Ndumbaro, Mei 23.
Waziri Ndumbaro amewaita Young Africans siku hiyo ambayo ndiyo atakuwa akiiwasilisha Bajeti ya Wizara yake katika Bunge hilo.