Boniface Gideon – Tanga.

Waziri wa Afya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga, Ummy Mwalimu, amewataka Wanawake na Vijana kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazowazunguka, ili kujikwamua kiuchumi, huku akitumia fursa hiyo kuwainua Wanawake wa Jiji la Tanga waliopo kwenye jukwaa la Wanawake Wilaya ya Tanga kwa kuwachangia Shilingi Milioni 5.

Akizungumza hii leo Mei 20, 2024 wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jukwaa la Wanawake Wilaya ya Tanga, ulioambatana na Uchaguzi wa Viongozi wapya, Waziri Ummy amesema huo ni wakati wa Wanawake kuamka na kuchangamkia fursa za kiuchumi, ikiwemo Mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa Makundi ya Wanawake, Wenye Ulemavu na Vijana.

Amesema, “Serikali imerejesha Mikopo ya Halmashauri ,na kuanzia Julai itaanza kutolewa,hivyo niwaombe Wanawake wenzangu tuchangamkie Mikopo hii, ili tukakuze Biashara zetu na tuondoe utegemezi kwa akinababa, na wanaochukua waache tabia ya kufanya anasa kwa kutumia fedha za Mikopo hiyo badala ya shughuli za kiuchumi.”

“jamani tuelewane,hii ni Mikopo na mkopo sharti lake ni lazima urejeshwe,msije mkachukua Mikopo alafu mkaenda kufanyia sherehe, lakini pia huko mtaani Kuna fursa nyingi sana, kwahiyo zichangamkieni na muwe wabunifu katika kazi zenu ili ziingie kwenye soko la ndani na Kimataifa,” amesisitiza Ummy.

Kwaupande wake Mkurugenzi wa Halmshauri ya Jiji la Tanga, Dkt. Frederick Sagamiko aliwataka Wanachama wa jukwaa hilo kuwa mfano kwa Wanawake wengine katika uwekezaji akisema Halmshauri imeweka mikakati dhabiti ya Mikopo ambayo itawanufaisha Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu.

Ubingwa wa Young Africans kwa Mkapa
Odegaard: Mafanikio ya ubingwa hayako mbali