Aliyewahi kuwa Mshambuliaji wa klabu za Chelsea na Manchester United Radamel Falcao ametangaza kuachana na Klabu ya Rayo Vallecano ya Hispania.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Colombia, amesema pamoja na kuachana na klabu hiyo, hana mpango wa kutangaza kustaafu soka na badala yake atatafuta klabu nyingine ili kuendelea kukipiga.
Mwishoni mwa juma lililopita Mshambuliaji huyo alihusishwa na mpango wa kuondoka Rayo Vallecano, licha ya kufahamika mkataba wake utafikia kikomo mwishoni mwa mwezi ujao, lakini yeye mwenyewe amethibitisha hilo hadharani.
Mshambuliaji huyo ambaye pia amewahi kuzitumikia klabu za Atlético Madrid (Hispania), AS Monaco (Ufaransa) na Galatasaray (Uturuki) amesema: “Mkataba wangu unaisha Juni 30 na kisha nitaangalia ni chaguo gani.
“Najisikia vizuri, nataka kuendelea kucheza, hivyo tutaangalia mpango huo kwa umakini, mimi na familia yangu ambayo ina uzito mkubwa katika uamuzi huu.
“Hakuna jambo ambalo limejadiliwa na klabu, kubaki kwenye La Liga ni jambo muhimu sana kwa Rayo Vallecano hasa kwa mashabiki wake, ambao huwa wanatupa ushirikiano kila mara, asante kwa miaka hii mitatu na ninawatakia Rayo mafanikio tele kwa siku zijazo. ”
Wakati huo huo Mtandao wa Diario Record umeripoti kuwa huenda Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 38 akahamia kwenye Ligi Kuu ya Soka nchini Mexico ‘Liga MX’.
Chanzo hicho kimeeleza: “Tunaweza kukuhakikishia kwamba watu wa karibu sana na Mcolombia huyo wanasema kwamba angefurahishwa na wazo la kucheza ‘Liga MX’.”