Scolastica Msewa – Pwani.
Serikali Nchini, imesema inaangalia namna bora ya kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakwamisha Wakulima na Wafanyabiashara sokoni kupima mazao yao kwa mizani badala ya kutumia Visado au makopo katika kumuhudumia jamii yaani mlaji wa mwisho.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoani Pwani, Hashimu Athumani wakati akitoa elimu kwa Wananchi na Wafanyabiashara wa soko la Loliondo na soko Jipya la Bagamoyo, juu ya matumizi ya Mizani ambao wameahidi kutumia Mizani na kuachana na matumizi ya vipimio visivyo rasmi.
Amesema, mkakati uliopo ni kuhakikisha upimaji wa bidhaa za mazao kuanzia kwa mkulima hadi kwa mfanyabiasha sokoni wanatumia mizani badala ya kutumia visado, makopo, ndoo au madebe ili kuwa na taifa ambalo mkulima, mfanyabiashara sokoni na mlaji wanapata faida.
“Changamoto zenu tunazipokea na tunazifanyia kazi kwa tafiti mbalimbali zinazoendelea kufanyika na tunaahidi kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili wote tunufaike na matumizi ya mizani na sio visado, makopo au ndoo. lazima tukubaliane kuuza kwa makopo, kununua kwa lumbesa iwe basi, ni lazima tukubaliane na utaratibu wa sheria ili za nchi na za kimataifa,” alisema Athuman.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Soko jipya la Bagamoyo, Yusuphu Athumani alishukuru Wakala hao kwa elimu aliyopata na kuahidi kuendelea kutoa elimu hiyo na kuwasimamia wafanyabiashara kutumia mizani kupima bidhaa zao.
Naye Meneja wa Kituo cha Wakala wa Vipimo Misugusugu, Charles Mavunde aliwataka wafanyabiashara na uuzaji wa mafuta kuzingatia sheria za nchi kwa kuhakikisha mitambo yao inahakikiwa na wakala huo kila mwaka, ili waweze kutoa huduma sahihi.