Kauli ya Rais wa Urusi, Vladmir Putin ya kusema kutakuwa na madhara makubwa iwapo nchi za Magharibi zitairuhusu Ukraine kutumia silaha zao kuyapiga maeneo ndani ya Urusi, huku akizionya nchi ndogo barani Ulaya kufahamu zinachokichezea kutokana na kuwa na maeneo madogo na idadi kubwa ya watu, inadaiwa imechangia mgawanyiko wa kimaamuzi wa Umoja Mawaziri wa Ulinzi wa umoja wa Ulaya.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amedai hakuna anayeweza kuzuia nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya kutoa silaha kwa Ukraine, ili kuzitumia kuyalenga maeneo ya kijeshi ndani ya Urusi na kwamba Mawaziri wa ulinzi wa umoja huo waliokutana jijini Brussels, wameshindwa kufikia makubaliano iwapo Ukraine inapaswa kuruhusiwa kutumia silahahizo.
Borrell anasema, Viongozi hao walikukubali kwa pamoja kutoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine lakini wakati baadhi yao wakitoa silaha kwa Kyiv kwa masharti, wengine wanadai huenda zikatumika ndani ya mipaka ya Ukraine ambayo inasema wanajeshi wake wanahitaji kuyapiga maeneo ndani ya Urusi inayoanzisha mashambulizi kutokea nchini mwake.
Ameongeza kuwa, mashambulizi ya kujilinda dhidi ya maeneo ya kijeshi katika ardhi ya Urusi ni kitendo halali chini ya sheria za kimataifa, iwapo yatatumiwa kwa ufasaha na kwamba kila mwanachama ana uamuzi binafsi wa kile anachoweza kuchangia na kushauri nini kifanyike ili mradi hawatovunja sheria husika.
Kwa upande wake Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron yeye anaunga mkono Ukraine kuruhusiwa kutumia silaha za Magharibi kuyashambulia maeneo ya Urusi, akidai ni muhimu kuviangamiza vituo vya kijeshi ambavyo vinatumika kufyatua makombora yanayoelekezwa ndani ya Ukraine.
Katika kauli yake, Putin alisema hata kama askari wa Ukraine watafanya mashambulizi hayo, wauzaji wa silaha kutoka nchi za Magharibi ndio watakaowajibishwa ambapo Nchi za Umoja wa Ulaya zikagawanyika pia kuhusu iwapo mafunzo ya kijeshi kutoka Umoja huo yanapaswa kuruhusiwa kutolewa kwenye ardhi ya Ukraine, au askari wa Ukraine wapelekwe katika Umoja wa Ulaya kwa zoezi hilo.