Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema Serikali imeamua kukarabati vituo vya Afya kongwe zaidi ya 200, vyenye miundombinu pungufu, ambavyo vinahitaji ukarabati mkubwa ili kuendana na mahitaji ya sasa ya utoaji wa huduma za afya.
Dkt.Dugange amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha Maswali na Majibu wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Esther Midimu aliyetaka kujua ni lini Serikali itajenga Jengo la OPD, katika Kituo cha Afya cha Kata ya Kiloleli, Wilaya ya Busega.
Akijibu swali hilo, Dkt. Dugange amesema, “Kituo cha Afya Kiloleli ni miongoni mwa vituo vya afya 202 kongwe na vyenye miundombinu pungufu, Serikali itavifanyia ukarabati na kujenga majengo muhimu katika vituo hivyo kwa awamu kikiwemo Kituo cha Afya Kiloleli katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega ambacho kitajengewa jengo la wagonjwa wa nje (OPD).”
Aidha, akijibu swali la , Mbunge wa Jimbo la Meatu, Leah Komanya aliyeuliza ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Maweni – Ng’hoboko – Meatu Dugange amesema, “katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali ilipeleka shilingi bilioni 1 katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Ilamba Ndogo na Mwasengela.
Ameongeza kuwa, “Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa awamu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata za kimkakati kote nchini. Aidha, Kata ya Ng’hoboko itajengewa kituo cha afya kwa kuzingatia mahitaji na vigezo vilivyoainishwa.”