Ukarabati wa Kivuko cha Mv. Magogoni unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Desemba, 2024 na kurejeshwa Nchini ili kuanza kutoa huduma kwa Wananchi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya Bungeni jijini Dodoma hii leo Mei 30, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndungulile aliyeuliza ni lini matengenezo ya Pantoni ya Mv. Magogoni iliyopo nje ya Nchi yatakamilika.
Februari 2023, Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania – TEMESA, ilisaini mkataba wa ukarabati wa kivuko cha Mv. Magogoni wenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.5.
Lengo la ukarabati huo wa Kivuko ni ni juhudi na mikakati ya Serikali katika kuboresha miundombinu mbalimbali ya usafirishaji, kuharakisha na kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi waishio katika Wilaya ya Kigamboni, Ilala na maeneo mengine.