Klabu ya Azam FC imejinasibu kuwa na hamu ya kulitaka Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘CRDBFC’ msimu huu 2023/24, ambapo mwishoni mwa juma hili watakuwa dimbani kutupa karata yao ya mwisho kwenye michuano hiyo.

Azam FC itapapatuana na Young Africans Jumapili (Juni 02) kwenye mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘CRDBFC’ katika Uwanja wa New Amani Complex Kisiwani Unguja-Zanzibar.

Afisa Habari wa Azam FC Hasheem Ibwe amesema dhamira yao kubwa ni kuhakikisha wanamaliza msimu wakiwa na taji mkononi, na taji lililosalia ni ‘CRDBFC’ pekee, baada ya mwali wa Ligi Kuu Tanzania Bara kurudi Young Africans.

Ibwe amesema ili kuifikia dhamira yao, kikosi chao kinapaswa kucheza kwa nidhamu kubwa kwenye mchezo huo ambao umepangwa kucheza mishale ya saa mbili usiku, kwa saa za Afrika Mashariki.

“Tunaliendea Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘CRDBFC’ kwenye Fainali kwa heshima adabu sana, kwa sababu tunajua aina ya timu ambayo tunakutana nayo huko, kwa hakika hautakuwa mchezo rahisi lakini tumejipanga kupambana na kufikia lengo tuliojiwekea.”

“Sisi tunachoamini sio kuhusu wao walivyo bali ubora wetu, hivyo tutaenda na adabu mno mbele yao kwa sababu tuna maandalizi mazuri na tumecheza vizuri karibuni na hatujakaa muda mrefu bila kucheza tunaamini ni sababu tosha ya kufikia lengo na kutwaa taji hilo,” amesema Ibwe

Azam FC ilitinga Fainali ya ‘CRDBFC’ kwa kuifunga Coastal Union ya jijini Tanga mabao 3-0 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, huku Young Africans wakiibutua Ihefu FC 1-0, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Jhonier Blanco mali halali Azam FC
Bajeti ya Wizara ya ujenzi kutekeleza vipaumbele tisa