Rais wa Ufilipino, Ferdinand Marcos Jr ameionya China kutovuka mstari mwekundu uliowekwa katika Bahari ya China Kusini, huku mzozo kati ya nchi hizo mbili ukiendelea kushika kasi.
Marcos ameyabainisha hayo wakati alipokuwa akizungumza kwenye kongamano la usalama nchini Singapore, lililohudhuriwa na wakuu wa ulinzi kutoka sehemu mbalimbali za dunia zikiwemo Uchina na Marekani.
Amesema, iwapo Mfilipino yeyote atafariki kutokana na hatua za makusudi za Uchina, watachukulia kuwa kitendo hicho ni vita na watajibu mapigo, huku Msemaji wa Jeshi la Uchina akiishutumu Ufilipino kwa shambulizi la maneno.
Katika miezi ya hivi karibuni, mzozo wa muda mrefu kati ya China na Ufilipino kuhusu eneo katika Bahari ya China Kusini umeongezeka baada ya Ufilipino kulalamika kuhusu meli za doria za China kurusha maji ya kuwasha kwenye boti za Ufilipino.