Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Geita ahakikishe analitokomeza kundi la kihalifu maarufu Mazombi, ambao wamekuwa wakiwasumbua Wananchi kwa kuwapora mali zao.
Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi katika Mji Mdogo wa Katoro Geita na kusema mazombi hayahitajiki, huku pia akiziagiza kamati za mazingira katika vijiji vyote zihakikishe maeneo yote ya vyanzo vya maji yanalindwa na kuzuia shughuli za kibinadamu zikiwemo za kilimo, ufugaji na ukataji wa miti ili kuepusha taifa kugeuka jangwa.
Awali, Mbunge wa Busanda, Tumaini Mageza aliishukuru Serikali kwa kuimarisha huduma za kijamii katika jimbo lao ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama ambapo hadi sasa tayari nyumba zaidi ya 200 zimeshaunganishiwa maji na vituo 10 vya kuchotea maji vimeanzishwa.
Mbunge huyo, alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali ianzishe mradi wa ujenzi wa shule za msingi za ghorofa kwa kuwa katika mji huo wanazaliwa watoto wengi kwa mwezi watoto 1,000 hivyo wakiendelea kujenga shule za kawaida watakosa maeneo.