Serikali imesema Timu ya wataalamu iko mbioni kukamilisha tathmini kuhusu mfumo endelevu wa usimamizi na uboreshaji wa mafao na pensheni kwa Wastaafu wanaolipwa na Hazina,
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024-2025 Leo Bungeni Jijini Dodoma na kudai kuwa pia Wizara imeendelea kulipa kwa wakati mafao ya wastaafu wanaolipwa na Hazina kila mwezi na kuwasilisha stahiki ya michango ya kisheria kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Aidha, katika hatua nyingine, Mwigulu amesema mkataba wa utozaji kodi mara mbili kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu umesainiwa na utekelezaji wake utaanza Januari 2025, ambapo kwa mwaka 2023/24, wizara ya fedha imehitimisha majadiliano ya mikataba minne ya utozaji kodi mara mbili kati ya Tanzania na nchi washirika.
Amezitaja nchi hizo kuwa ni ni Jamhuri ya Czech, Jamhuri ya Kisultani ya Oman, Jamhuri ya Iran na mkataba wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo hatua za kusainiwa kwa mikataba hiyo zinaendelea.
Mwigulu amesema, “manufaa ya kuhitimishwa na kusainiwa kwa mikataba hiyo ni kuondoa vikwazo vya kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi husika, kuvutia mitaji kutoka nje, kuongezeka kwa fursa za ajira, kupanua wigo wa fursa za kibiashara na soko la malighafi, bidhaa na huduma zinazozalishwa na wawekezaji wa ndani.”