Lydia Mollel – Morogoro.
Mradi wa USAID Kizazi Hodari chini ya usimamizi wa Kanisa la ELCT unalenga kuwafikia watoto zaidi ya laki moja kwa ajili ya kuboresha afya, ustawi wa jamii na lishe kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Watoto hao ni wale waliopo kwenye hatari ya maambukizi ya VVU na wanaoishi kwenye kaya za wazazi/walezi wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi, kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kupata huduma muhimu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mshiriki wa USAID Kijana Hodari Issa Mushid katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya Mkoani Morogoro, ili kuwasilisha na kubadilishana takwimu za utekelezaji wa kazi kwa kipindi cha robo mwaka pamoja na kubadilishana ujuzi.
Mushid amesema mradi huo umejikita kuhakikisha kaya zao zinaimarishwa kiuchumi kwani kuna uhusiano mkubwa kati ya uchumi mbaya na maambukizi ya VVU.
Josphine Mwaipopo, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dodoma, amesema mradi huo umesaidia serikali kupata takwimu za watoto waliotambuliwa pamoja na changamoto wanazokutana nazo, kwani zitawasaidia kupanga mipango ya mwaka na kuweka mikakati mbalimbali ya kutokomeza ukatili kwa watoto.