Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo kuhakikisha kuwa biashara katika soko la Kariakoo zinafanyika saa 24 pindi ujenzi wa soko hilo utakapokamilika.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo Julai 5, 2024 wakati wa hafla ya uapisho wa viongozi wateule iliyofanyika Ikulu ndogo ya Tunguu huku akimtaka Waziri Jafo pia afanye kazi kwa ukaribu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Mipango na Uwekezaji pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ili kusimamia sekta ya biashara katika soko hilo.
Aidha, Dkt. Samia pia amemtaka Waziri Dkt. Jafo kuhakikisha kunakuwa na mahusiano mazuri baina ya wafanyabiashara na Serikali kote nchini pamoja na kutatua kero zao, hali itakayopelekea Serikali kukusanya mapato stahiki na wafanyabiashara kunufaika na biashara zao.
Katika kuhakikisha raia wa kigeni hawajihusishi na biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa, Rais Dkt. Samia amemuelekeza Waziri Dkt. Jafo kufuatilia utoaji wa leseni kwa wazawa na wageni ikiwa ni pamoja na kusajili wafanyabiashara na kuwa na kanzidata yao.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amemtaka Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kuongeza mapato ya ndani yatakayowezesha Serikali kutoa huduma kwa wananchi kupitia mapato hayo.
Amemuagiza Kamishna Mwenda kuhakikisha mifumo ya TEHAMA kati ya TRA na Mamlaka ya Bandari inasomana ili kuweza kukusanya kodi itakayosaidia kuwekeza katika miradi ya maendeleo na amemuelekeza kuhakikisha wafanyabiashara wote nchini wanatumia Mashine za Kielektroniki (EFD) na kuwahamasisha wananchi kudai risiti kwa manunuzi wanayofanya.