Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa wa kiuchumi (GEF) imezipongeza taasisi zinazowezesha upatikanaji wa haki za wanawake na watoto Zanzibar kwa jitihada zake za kukuza haki na usawa wa kiuchumi kwa makundi yote.
Pongezi hizo zimekuja kufuatia ziara ya kamati hiyo kutembelea taasisi za Mwanamke Initiatives Foundation (MIF), na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) iliyolenga kufuatilia utendaji wa taasisi hizo katika kuchangia ufikiaji wa kizazi chenye Usawa wa Kiuchumi.
Abeida Rashid Abdallah, mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar alisema taasisi hizo zinafanya kazi kubwa ya kuisaidia serikali kufikia malengo yake ya kujenga kizazi chenye usawa wa kiuchumi kwa wanawake.
Alieleza, “tumefurahishwa sana na tumeona kazi kubwa inayofanywa na taasisi hizi katika kukuza haki na usawa wa kiuchumi kwa kuwajengea uwezo wanawake kuzifikia fursa mbalimbali za kiuchumi.”
Alishauri licha ya juhudi kubwa kuchukuliwa lakini bado wanawake wengi wanakabiliwa na tatizo la udhalilishaji wa kiuchumi na kuzitaka taasisi hizo kuendelea kuweka mkazo kwenye elimu ya kupinga udhalilishaji wa kiuchumi katika shughuli zao.
Naye Mohamed Jabir, mjumbe wa kamati hiyo alisema kamati imeridhishwa zaidi na namna ambavyo taasisi hizo hasa TAMWA ZNZ imesaidia kuwaondoa wakulima wa viungo kutoka kwenye kilimo cha mazoea hadi kilimo cha kibiashara.
“Wametuonesha ni namna gani TAMWA ZNZ wanachukua juhudi za serikali kusaidia kufikia malengo yake ya kizazi chenye usawa wa kiuchumi hasa kwa kuwawezesha wanawake kwenye kilimo biashara cha Viungo,” alieleza Jabir.
Kwa upande wake Mwajuma Magwiza, alizishauri taasisi hizo kubuni vipaumbele vipya vya kuwawezesha wanawake kuzifikia fursa zaidi za kiuchumi hasa kwenye sekta ya utalii.
Magwiza alisema, “nashauri hizi taasisi zinazotoa elimu ya ujasiriamali ziongeze kipengele cha kuwafundisha lugha wajasiriamali ili wawe na uwezo wa kuzungumza na watu mbalimbali bila kiwazo kwani tumeona licha ya kazi kubwa wanayofanya bado lugha ni changamoto kwa wanawake wajasiriamali wengi.”
Katika hatua nyingine, Abdallah Duchi mmoja wa wajumbe GEF walioshiriki ziara hiyo alitaja miongoni mwa mapungufu yaliyobainika ni kutokuwepo kwa mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu kuzifikia fursa zilizopo.
“Taasisi za kutoa huduma zinapaswa kuboresha mazingira yake ili kuwezesha ufikiaji wa makundi yote hasa watu wenye ulemavu kwasababu maeneo mengi tuliyofika hata ofisi zake bado hazijazingatia watu wenye mahitaji maalumu kufika bila kikwazo,” alieleza, Abdallah Duchi.
Mapema afisa uwezeshaji wanawake kiuchumi wa TAMWA ZNZ, Nairat Abdalla, aliieleza kamati hiyo kuwa mradi wa Viungo ulilenga kuwawezesha wanawake kukuza uchumi kupitia kilimo cha kisasa ambapo zaidi ya wanawake 2,000 wamefanikiwa kuzalisha mazao mbalimbali ikiwemo Vanilla.
Kamati hiyo katika ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa Zanzibar imefanikiwa kutembelea taasisi za umma na binafisi, ikiwemo vikundi vya wanawake wajasiriamali wanaotekeleza afua za kizazi chenye Haki na Usawa wa Kiuchumi.