Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kufungua Mkoa wa Katavi kwa kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.
Rais Dkt. Samia ameeleza hayo leo Julai 15, 2024 Mkoani Katavi wakati akihitimisha ziara yake Mkoani humo na kukagua mradi wa barabara ya Kibaoni – Sitalike (km 74) sehemu ya Kibaoni – Mlele (km 50) inayojengwa kwa kiwango cha lami.
“Niwaahidi wana Katavi jicho la Serikali lipo katika Mkoa huu, Lengo ni kuufungua Mkoa wa Katavi kwa njia zote na kama mnavyojua Bandari ya Karema tumeshaimaliza na imeanza kazi na sasa tunaenda kujenga barabara inayounganisha Bandari hiyo ili kufikisha bidhaa na mazao katika Soko”, amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia ameeleza kuwa amesikia kilio cha kuchelewa kwa ujenzi barabara ya Kibaoni – Mlele (km 50) ambao ujenzi wake umefika asilimia 15 wakati mpango kazi ilitakiwa kufika asilimia 30 na kuahidi kuikamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa mtandao wa barabara unaosimamiwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Katavi kwa kipindi cha miaka 12 umeongezeka kutoka kilometa 1.9 hadi kufika kilometa 340 za barabara kwa kiwango cha lami.
Aidha, Bashungwa amemuhakikisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wananchi wa Mpimbwe kuwa ujenzi wa barabara ya Kibaoni – Mlele utekelezaji wake utaaanza kwenda kwa kasi ile inayotakiwa baada ya kufanyia kazi changamoto zilizokuwa zinamkabili Mkandarasi huyo.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zile changamoto za kifedha ambazo zilikuwa zinafanya Mkandarasi kusuasua tumezifanyia kazi na ulituelekeza kuongeza bajeti ya kutosha kwenye barabara ya Kibaoni – Mlele katika Bajeti mpya ya Serikali inayoanza mwezi Julai mwaka huu ili Mkandarasi aongeze spidi ya ujenzi”, amekaririwa Bashungwa.
Bashungwa ametaja hatua nyingine iliyochukuliwa na Wizara ya Ujenzi kwa Mkandarasi huyo anayeteleleza ujenzi wa barabara ya Kibaoni – Mlele ikiwa ni pamoja na kutomuongezea miradi mingine mipya hadi akamilishe ujenzi wa barabara hiyo.
Vilevile, Bashungwa ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi imepokea Shilingi Bilioni 6.7 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Daraja la Mirumba lenye urefu wa mita 60 na tayari Mkandarasi ameshaanza maandalizi ya kuanza ujenzi na muda sio mrefu kazi ya utekelezaji itaanza.
Bashungwa ameeleza kuwa zimebakia kilometa 84 kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma kupitia Uvinza na Wakandarasi wapo wanaendelea na kazi usiku na mchana.