Hatimaye maandamano ya amani yamerejea kote nchini Kenya, yakishinikiza uwajibikaji na kuwakumbuka waliouawa katika wiki tatu za kupinga Mswada wa fedha wa 2024 uliotupiliwa mbali na Seri ya nchi hiyo.
Hali hiyo imeendelea kuleta hofu katikati ya jiji la Nairobi ambako maduka yamefungwa na idadi ya watu wanaotembea ikiwa ni chache kuliko ilivyozoeleka huku baadhi ya barabara zikifungwa.
Hata hivyo, Kaimu Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja amewatahadharisha waandamanaji na wahalifu wanaopanga kuvuruga amani akiwataka kushirikiana na maafisa wa usalama.
Haya yanajiri baada ya miili zaidi ya nane kuopolewa huko Kware mtaa wa Embakasi huku familia zikiombwa kujitokeza kutambua maiti hizo ambazo zinafanyiwa ukaguzi na upasuaji kwenye kituo cha Jiji.
Tayari Baraza la Makanisa limelaani mauaji na kuelezea kuwa yanakiuka sheria. Askofu Antony Muheria ni wa kanisa la katoliki dayosisi ya Nyeri na anaamini ipo nafasi ya kufanya mabadiliko.
Muswada wa fedha wa 2024 wa Kenya, ulitarajia kukusanya dola bilioni 2.7 za Marekani za Pato la ziada katika mwaka mpya wa fedha ikiwa ni baadhi ya masharti ya IMF jambo ambalo liliamsha hisia kali za waandamanaji wanaopinga.