Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imejenga Hospitali za kisasa na kwa gharama kubwa, ili kuzuia Watanzania kwenda nje ya Nchi.
Dkt. Samia ameyasema hayo akiwa Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe hii leo Julai 18, 2024 na kudai kuwa Hospitali hizo zile kuanzia ngazi za Wilaya kwenda Rufaa na kwamba matibabu yana gharama hivyo Watanzania ni lazima wachangie huduma za afya kwa kukata Bima za afya.
“Maendeleo yakifanywa huzaa maendeleo mengine Serikali imejenga Hospitali maeneo yote pamoja na Rufaa ,Sasa Hospitali hizi ndani ya mikoa ni Hospitali za Kisasa huku lengo ni kuzuia watanzania kupelekwa nje kwa matibabu labda tatizo liwe kubwa sana tumelishindwa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amemuondolea gharama zote za matibabu Mama aliyejitokeza katika mkutano wake wa njiani wakati akiwasalimia Wananchi wa Mlowo Wilaya Mbozi Mkoa Songwe kuelekea Dodoma .
Rais amemuagiza Naibu wa waziri wa Afya, Dkt Godwin Mollel ahakikishe Mama huyo aliyesema mtoto wake ana tundu la moyo pia na mirija yakusafirisha damu safi na salama imeungana huku gharama za matibabu ikiwa ni milioni nane laki nane na elfu hamsini atibiwe haraka.
“Mtoto atibiwe Kadri kadri tutakavyoweza ,ninachotaka mtoto atibiwe,” alisema Dkt. Samia