Lydia Mollel – Morogoro.

Ugumu wa maisha umemfanya mkazi wa kitongoji cha Lukobe Juu Manispaa ya Morogoro, Evelina Sales kushindwa kumpeleka mwanae kupata matibabu baada ya mumewe kumkimbia na kutelekeza familia yake isiyokuwa na kipato.

Mwanae  huyo mwenye umri wa mwaka mmoja na Miezi 6, alizaliwa na changamoto ya kupata haja ndogo na hivyo kupasuliwa ubavuni  kupata sehemu ya kutolea haja kubwa.

Evelina, anaeleza kuwa mtoto huyo alizaliwa akiwa na hilo tatizo katika hospital ya Mkoa wa Morogoro na kupewa rufaa ya kwenda Muhimbili na alishindwa kufanyiwa upasuaji mkubwa kutokana na kukosa fedha za matibabu jambo ambalo lilimlazimu kurudi nyumbani huku akiacha deni la  shilingi laki nane.

Anasema,” baada ya kurudi kutoka Hospitali nilikuta pale tulipokuwa tunaishi kuna deni kubwa sana ambalo nisingweza kulipa, lakini Muhimbili pia nadaiwa laki nane Mume wangu alikimbia bila kulipa, yule mwenye nyumba akatufukuza, katika kuzungumza na watu nikawaeleza hali ninayopitia akatokea msamaria mwema akaniambia yeye anayo nyumba yake aijakamilika atanipa niishi hapo.”

Evelina anaongeza kuwa, “akanipa hii nyumba tunayoishi kwa sasa kwani sina uwezo wa kifedha kumudu maitaji muhimu inabidi niishi hapa hadi mwanangu atakapo.”

Polisi Kata wa Kata ya Lukobe, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi ,Zuena Mwita amesema akiwa anatekeleza majukumu ya utoaji elimu alifuatwa na mama huyo na kumuomba amsemee kwenye jamii, ili apate msaada na aweze kwenda hospitali.

“Nilikuwa kwenye harakati zangu za kutoa elimu kwa jamii,ndipo mama huyu akanifata na kunieleza changamoto anayopitia mwanae,bila kusita nilifika nyumbani kwake nakumuona mtoto huyu, kiukweli mtoto anahitaji matibabu ya haraka ni mdogo, nilichofanya niliomba wadau angalau apate kwanza mahitaji muhimu naombeni Watanzania mumsaidie angalau na yeye aje atimize ndoto zake,” alisema Mwita.

Naye Mwenyekiti wa mtaa huo, Tekla John amesema kuwa changamoto ya mama huyo wanaijua na washafanya jitihada za kumsaidia ambazo hazikuzaa matunda kutokana na hali ngumu waliyonayo hivyo kama kuna yaeyote atakayeguswa anaweza kumsaidia au kuwasiliana naye kwa kutumia namba 0655710630.

Kenya: Mahakama yabatilisha marufuku ya maandamano
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Julai 19, 2024