Bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi – PSPTB, imetangaza rasmi matokeo ya mitihani ya 28 ya PSPTB iliyofanyika Mei 13 hadi Mei 17 2024 katika vituo 6 vya Tanzania bara na visiwani
Akizungumza na vyombo vya habari hii leo Julai 19, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji, Godfrey Mbanyi amesema jumla ya watahiniwa 1280 walisajiliwa, ili kufanya mitihani, watahiniwa 1197 sawa na asilimia 93.5 walifanya mitihani na kwamba hilo ni ongezeko ukilinganisha na msimu uliopita uliokua na watahiniwa 977.
Amesema, kati ya watahiniwa 1280, watahiniwa 551 sawa na asilimia 46.0 wamefaulu, 632 sawa na asilimia 52.8 watarudia baadhi ya masomo kuanzia 1 hadi 3 kutegemeana na aliyofeli, huku watahiniwa 14 sawa asilimia 1.2 wamefeli masomo yote.
Aidha, katika masomo 39 waliopimwa watahiniwa ni masomo 24 yamefanywa vizuri, 07 yamefanywa kwa wastani, 08 wamefeli. Na kwamba wanawake wamefanya vizuri zaidi kuliko wanaume, watahiniwa 2 wa kike waneibuka bora katika ngazi ya Graduation Professional 1 na CPSP.
Mbanyi amefafanua kuwa mikakati iliyowekwa na PSPTB ni kuendelea kuimarisha na kusimamia ubora wa mafunzo yanayotolewa na vituo vya kuwaandaa watahiniwa, kuimarisha mahusiano ya kitaaluma na taasisi za elimu ya juu na kati.
Amesema lengo ni kuendeleza ubora na ufaulu wa mitihani ya PSPTB, kusimamia na kuhimiza uanzishaji wa mafunzo kwa kutumia fursa za mitandao zilizopo na kuendelea kufanya ziara za mafunzo vyuoni na katika vituo vya mafunzo vilivyosajiliwa na PSPTB.