Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameilekeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kukamilisha Mwongozo wa Utambuzi wa Machifu na Viongozi wa Kimila katika Wilaya na Mikoa utakaoainisha majukumu yao wa kimila na kijadi.
Rais Dkt. Samia ametoa maelekezo hayo hii leo Julai 20, 2024 wakati akizungumza na Viongozi wa Kimila na Machifu kutoka Tanzania nzima kwenye hafla iliyofanyika Ikulu, Chamwino jijini Dodoma.
Amesema Viongozi wa Kimila na Machifu wana mchango mkubwa katika kulinda maadili na kutatua changamoto za kimaadili katika jamii licha ya kuwa yanashughulikiwa katika ngazi ya Serikali.
Rais Dkt. Samia pia ametoa rai kwa Machifu kote nchini kuendelea kujenga mvuto na uaminifu wa watu ili waweze kutoa mchango wao ipasavyo kwa ushrikiano na Serikali katika utatuzi wa migogoro inayoikabili jamii.
Aidha, amekemea vitendo vya utekaji na mauaji ya watoto kwa imani potofu za ushirikina ambayo ni kinyume cha maadili ya Watanzania na kuwasihi Machifu na wananchi wote kukemea vitendo hivyo.
Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara hiyo kuimarisha michezo ya Umoja wa Michezo ya Shule za Msingi na Sekondari (UMISSETA na UMITASHUMTA) ikiwa ni sehemu ya kuwafundisha na kudumisha mila na desturi.
Amesema dunia inaposhuhudia mabadiliko mbalimbali, Serikali ya Tanzania itahakikisha kuwa inashuhudia maendeleo ambayo yanadumisha mila na desturi za Watanzania.