Katika kuelekea Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kimataifa ya Homa ya Ini, Serikali Nchini imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti ugonjwa huo, kwa kuendelea kujumuisha huduma za homa ya ini na magonjwa ya ngono.

Magonjwa hayo ni yale yaliyokuwa kwenye uliokuwa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ugonjwa wa UKIMWI (NACP) pamoja na Kuimarisha upatikanaji wa chanjo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Akizungumza Jijini Dodoma hii leo Julai 24, 2024 Mkuu wa Programu za UKIMWI, Ngono, Ini, Malaria, Kifua Kikuu, Uelimishaji mifumo ya afya, Dkt. Catherine Joakim amesema pia Serikali imeendelea kuelimisha Wananchi kuhusu ugonjwa wa homa ya ini Mijini na Vijijini.

Amesema, “Napenda kutoa rai kwa wananchi kutumia fursa ya huduma hizi kwa kupata huduma za kujikinga pamoja, uchunguzi na tiba, hata hivyo takwimu za Shirika la Afya Duniani za mwaka 2021 zinaonyesha kuwa Duniani kuna watu wapatao milioni 296 ambao wanaishi na maambukizi  sugu ya Virusi vya Homa ya Ini aina B.”

Dkt. Catherine ameongeza kuwa “watu milioni 58 wanaishi na  maambukizi  sugu ya Virusi vya Homa ya Ini aina C. Barani Afrika kuna Watu milioni 60 wanaishi na maambukizi  sugu ya Virusi vya Homa ya Ini aina B na Watu milioni 10 wanaishi na  maambukizi  sugu ya Virusi vya Homa ya Ini aina C. Hapa nchini inakadiriwa kiwango cha ushamiri wa ugonjwa wa Homa ya Ini ni asilimia 3.5 (aina B) na asilimia 1 (aina C)”

Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kimataifa ya Homa ya Ini yamepangwa kufanyika Sinza darajani, Uwanja wa TP Jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 25-28, 2024 ambapo Mgeni rasmi anatarajia kuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Mpango kupunguza vihatarishi vya maafa wazinduliwa
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Julai 24, 2024