Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Charles Mahera amewaelekeza Makatibu wa Afya Mikoa na Halmashauri nchini kufuatilia, kushughulikia na kutatua kero za watumishi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe ili waweze kufanya kazi zao za kuwahudumia wananchi.
Kauli hiyo imetolewa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afya ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Subisya Kabuje tarehe 23 Julai, 2024 mkoani Kigoma wakati akiongea na timu ya usimamizi wa huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika ziara ya siku mbili inayoendelea mkoani humo.
Amesema watumishi wa Afya ngazi ya vituo vya afya na zahanati wamekuwa na changamoto nyingi ambazo zinawakwamisha katika utekelezaji wa majukumu yao kila siku katika kuwahudumia wananchi hivyo zinapaswa kutatuliwa. Huku akitaja miongoni mwa changamoto hizo ni upandishwaji wa madaraja kwa watumishi wa Sekta ya Afya.
Amemtaka Afisa maendeleo ya jamii wa Manispaa ya Kigoma mjini kusimamia kwa ukaribu vikundi vya walemavu katika Halmashauri hiyo ambao ni wanufaika wa mikopo ya 10% itokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri, amesema hayo baada ya kutembelea katika kikundi cha walemavu cha Nia njema.
Subisya amesema, “Kikundi cha walemavu cha Nia Njema kimekuwa ni mfano wa kuigwa kwani ni miongoni mwa vikundi vichache ambavyo vinachukua Mkopo ya 10% ya mapato ya Halmahauri na kurejesha kwa wakati uliopagwa na wao kuendelea na shughuli za uzalishaji. Hivyo Afisa maendeleo ya Jamii unapaswa kuongeza usisimamizi wa karibu katika vikundi vya namna hii ili viweze kufanya vizuri zaidi.”
Aidha, amewaelekeza watumishi wa Afya ngazi ya mkoa (RHMTs) na Halmashauri (CHMTs) kuwa na tabia ya kushuka chini kwenye ngazi ya jamii na kusaidiana na wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii (CHW) kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Damas Kayera amesema ameyachukua maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kama ambavyo imeelekezwa.