Vitendo vya kishirikina, visasi, hali ngumu ya maisha, biashara haramu, ukosefu wa elimu, kuporomoka kwa maadili na tamaa ni miongoni mwa vyanzo vya matukio ya watu wanaodaiwa kupotea au kutekwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamebainishwa na Wadau wa Jinsia na Maendeleo Jijini Dar es Salaam katika Semina za Jinsia na Maendeleo zinazofanyika kila Jumatano katika Viwanja vya TGNP- Mtandao huku ikihusisha wadau mbalimbali wa Maendeleo.
Akizungumza katika Semina hiyo, Mkazi wa Manzese, Hamisi Masanja amesema kwa sasa ushirikiano kutoka kwenye vyombo vya ulinzi wa raia na mali zao ni mdogo kwani ushirikiano huo ungekuwepo masuala haya ya utekaji wa watoto usingekuepo.
Amesema, “ni vyema kikosi cha polisi kifanye kazi yake na wananchi kutoa ushirikiano pale utekaji unapitokea. kitu kikitendeka kwanza kitilie hamu kukifahamua kama unaona kinahitaji msaada toa msaada hatakama wa kupiga kelele ili kuokoa maisha yale muhusika.”
Naye mkazi wa Makulumla Mpegwa Noa amesema masuala ya utekaji wa watoto wazazi wengi wanalalamika hivyo ameiomba serikali kufatilia watekaji hao na kuwachukulia sheria stahiki ili kukomesha mauaji na utekaji ambao umeenea katika baadhi ya maeneo nchini.
Ili kuondokana na hali hiyo, wadau hao wamesema jamii natakiwa kuwa na moyo wa imani, kuwepo kwa ushirikiano, kukamata waganga wasio na vibali, elimu iongezwe kwenye jamii, makanisa na misikiti yasiyo na mafundisho mazuri yadhibitiwe , malezi bora na kuwakumbusha watoto wajibu wao, vyombo vya dola kutimiza majukumu yake.