Angela Msimbira, Kaliua – Tabora.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu), Zainab Katimba amezielekeza halmashauri zote nchini zinazotekeleza miradi ya ujenzi wa shule mpya maalum za wasichana za mkoa kuhakikisha wanaongeza usimamizi wa mradi hiyo ili kuendana na thamani ya fedha.
Ametoa maelekezo hayo wakati alipotembelea shule maalum ya Wasichana ya Mkoa wa Tabora iliyojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora huku akiwataka viongozi hao kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na inajengwa kwa ubora ili dhamira ya serikali ya awamu ya Sita ya kuhakikisha watoto wa kike wanasoma masomo ya sayansi katika mazingira bora na tulivu inatimia.
Amesema Rais Samia anatafuta fedha za kujenga shule maalum za sayansi za wasichana kila mkoa ili kuwawezesha kupata miundombinu bora itakayokuwa chachu kwa watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi
Pia amewataka viongozi hao kuhakikisha wanatumia miongozo iliyotolewa na serikali katika utekelezaji wa mradi huo ambayo ilitolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili shule hizo ziweze kujengwa kwa utaratibu uliowekwa na serikali.
Amewataka pia kuhakikisha ujenzi wa shule hizo unaenda sambamba na utunzaji wa mazingira kwa kutunza miundombinu iliyojengwa ili iweze kutumika kwa vizazi vingi zaidi.
Aidha, Katimba amewaasa wanafunzi wa shue ya Sejondari Batilda Burhan kuzingatia masomo ili wamalize shule salama na baadaye wawe na maisha bora yaliyochagizwa na miundombinu bora ya elimu ambayo imejengwa na Rais Samia ambaye tangu aingie madarakani alidhamiria kuwapatia fursa watoto wa kike ya kupata elimu bora.
“Msichanganye elimu na mambo mengine yatakayowakwamisha kutimiza ndoto zenu za kuwa wahandisi, madaktari, marubani na wanasayansi mnaotegemewa nchini na kwenye mataifa mengine,” amesisitiza Katimba.