Watu 21 wamefariki ndani ya saa 24 katika mji wa Beni Mellal, uliopo katikati mwa Morocco, kutokana na joto linaloikumba nchi hiyo katika kipindi cha mwaka wa sita mfululizo wa ukame.
Taarifa ya Kurugenzi ya Wizara ya Afya nchini humo imeeleza kuwa idadi kubwa ya watu waliokufa ni wale wanaougua magonjwa sugu na wazee huku joto la juu likichangia kuzorota kwa hali za walionusurika ambao wanaendelea kupatiwa matibabu.
Aidha, hatua za kukabiliana na athari za joto hilo zimeanza kuchukuliwa kuanzisha saa za kudumu ndani ya vituo vya afya katika mikoa iliyoathiriwa, pamoja na uhamasishaji wa wataalamu wa afya na utoaji wa dawa na vifaa vya kusaidia kujikinga na adha hiyo.
Hata hivyo, utabiri wa Mamlaka ya hali ya hewa nchini humo – DGM unaonesha kuwa hali ya joto inatarajiwa kushuka katika siku zijazo huku ikionekana kuwa mji wa Marrakech (kusini), hali ya joto ilifikia digrii 45 siku ya Alhamisi Julai 25, 2024 na itapungua kwa digrii 10 siku ya Jumapili Julai 28, 2024.