Kuelekea kilele cha wiki ya Wananchi klabu ya Yanga imeendelea na kampeni zake za kurudisha kwa jamii na leo hii uongozi na mashabiki wa klabu hiyo walitembelea hospitali ya mkoa wa temeke kwa shuguli mbalimbali ikiwemo usafi na kutoa misaada ya vitu mbalimbali.
Kundi hili la mashabiki liliongozwa na Afisa Habari wa klabu hiyo Ally Kamwe wadhamini wa klabu hiyo GSM FOUNDATION,CRDB na Sport Pesa. Yanga imekuwa na utaratibu wa kuwafikia watu wenye uhitaji maalumu ikiwa ni sehemu ya kukumbuka michango yao kwa klabu hiyo.
Zoezi la misaada liliambatana na usajili wa wanachama wapya wa klabu hiyo, usambazaji wa tiketi za kuingia uwanjani siku ya kilele cha wiki ya wananchi siku ya jumapili tarehe 4 Agosti.
Kwa upande wa watani zao wa jadi klabu ya Simba siku ya jana wakiongozwa na Afisa habari wa Klabu hiyo Ahmed Ally walifanya kampeni ya kuchangia Damu na kutoa misaada mbalimbali kwa wanafunzi wa shule ya viziwi Buguruni. Kampeni hizo ziliambatana na wadhamini wa klabu hiyo M BET na MO DEWJI foundation.
maafisa habari Ahmed Ally na Ali Kamwe wamefanya kazi kubwa ya kuwakutanisha mashabiki wa klabu hizo na kuimarisha uhusiano baina ya viongozi na mashabiki hao. kwa upande mwingine maafisa habari hao wamefanikisha kwa kiasi kikubwa mauzo ya jezi na uuzaji wa tiketi.
Klabu hizo zitahitimisha wiki zao kwa kukutana na mashabiki wao kabla ya msimu kuanza siku ya Jumamosi na Jumapili. Tarehe 8 Agosti watachuana kwenye mchezo wa nusu fainali ya kombe la Community Shield.