Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni – NCMC, kimeshauriwa kupanua wigo wa utoaji wa elimu kuhusu fursa na manufaa ya biashara hiyo kwa wananchi.

Ushauri huo umetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya), Dkt. Festo Dugange alipotembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma.

Amesema iwapo elimu ya kutosha kuhusu biashara ya kaboni itatolewa kwa wananchi hususani kupitia fursa ya upandaji miti itasaidia uelewa kuhusu uhifadhi wa mazingira na kuongeza kipato katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.

Dkt. Dugange amesema zipo baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatekeleza miradi ya biashara ya kaboni na hivyo kutoa ushauri kwa Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni (NCMC) kubuni na kuweka mipango mahsusi ya kushirikiana na Halmashauri hizo katika utoaji wa elimu.

“Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) hakina budi kujitangaza ili kiweze kufahamika na kufikia wadau wengi ikiwezekana hata kufungua ofisi za Kanda katika Mikoa mbalimbali nchini”.

Amesema ni wakati mwafaka kwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu ya biashara ya kaboni inatolewa kwani bado jamii haina hawana uelewa wa kutosha kuhusu kaboni pamoja na fursa na faida zilizopo katika biashara hiyo.

Pia aliitaka Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia NCMC kufanya mikutano na makongamano na wadau ili kutoa elimu kwa ikiwemo wananchi na taasisi mbalimbali za uwekezaji ambao ndio walengwa wakubwa wa biashara ya kaboni nchini.

Ziara Moro: Rais Samia ateta na Wananchi Ifakara
100 wafariki kwenye maandamano, Jeshi latoa kauli