Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali imejipanga kurejesha ile hadhi ya kihistoria ya Mkoa wa Morogoro kuwa mkoa wa viwanda kwa kufufua viwanda na kuvutia uwekezaji mpya.
Rais Samia ameyasema hayo wakati akihutubia wakazi wa Mkoa wa Morogoro katika Uwanja wa jamhuri akihitimisha ziara yake ya siku 5 kwenye Mkoa huo.
Amesisitiza kuwa uwepo wa miundombinu ya reli na uwepo wa umeme wa uhakika kutoka Bwawa la Julius Nyerere unaufanya Mkoa wa Morogoro kuwa sehemu nzuri kwa uwekezaji.
Katika ziara yake Mkoani humo Rais Samia alitembelea uwekezaji wa upanuzi wa viwanda uliofanywa Mkoani humo ikiwemo Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa na Kiwanda cha Sukari cha Kilombero.
Pamoja na mambo mengine, Rais Samia amesema kuwa upanuzi huo wa uwekezaji kwenye viwanda unampa imani kuwa ifikapo mwaka 2025/2026 Tanzania itakuwa katika nafasi nzuri ya kujihakikishia uzalishaji wa sukari kukidhi mahitaji yake.
Rais Samia pia amesema kuwa uwezekaji huo na upanuzi wa viwanda vilivyopo ni ishara kuwa Tanzania ina mazingira bora na yanayovutia kwa uwekezaji wa viwanda ns kutoa rai kwa wakulima kuendelea kuzalisha kwa wingi ili kulisha viwanda vinavyojengwa.
Rais Samia pia alizindua Kiwanda cha Sigara cha Serengeti (SCC) katika eneo la Kiwanda cha Uchakataji Tumbaku cha Mkwawa (MTPL) ambapo amepongeza uwekezaji huo ambao utakamilika Juni 2025, na kuzalisha ajira mpya 12,000 Mkoani Morogoro.