Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi – CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemuagiza Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki kuifanyia kazi na kupata ufumbuzi wa changamoto ya wanyama waharibifu wanaovamia makazi ya watu, kuharibu mazao na kutishia uhai wa binadamu, Wilaya ya Karagwe.

Balozi Dkt. Nchimbi pia amezielekeza mamlaka husika mkoani Kagera, kwa kushirikiana na wizara za kisekta husika, kushughulikia na kumaliza tatizo la matumizi ya ardhi, mipaka kati ya wananchi na Kampuni ya Ranchi za Taifa NARCO, Wilayani Karagwe.

Ametoa maelekezo hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kituco cha Mabasi cha Kayanga, Wilayani Karagwe, mkoani Kagera, akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya siku sita mkoani humo, ambapo miongoni mwa kero za wananchi wa jimbo alizotaarifiwa, ni pamoja na uvamizi wa wanyama hao wakali katika vijiji vya Kata ya Kihanga (Kihanga, Kibwela na Mshabaiguru), ambako Tembo wanavamia mashamba ya wakulima, kuharibu mazao na kuhatarisha maisha wa wananchi katika maeneo husika.

Pia, alitaarifiwa kuhusu uwepo wa mgogoro wa ardhi Kata ya Rugera, kati ya wananchi na Shirika la NARCO katika Kijiji cha Omukakajinja, ambapo alitoa maelekezo, kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kuziagiza mamlaka zinazohusika, zikiwemo za kisekta, kufanyia kazi masuala hayo na kumpatia taarifa za kumalizika kwa migogoro hiyo.

Balozi Dkt. Nchimbi ametaka changamoto hiyo ishughulikiwe haraka ikiwemo kutafuta namna ya kudhibiti wanyama waharibifu hasa Tembo lakini pia suala la mipaka ili ijulikane.

Katika hatua nyingine Balozi Nchimbi amemshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa kuusikia wito wa suala la Vitambulisho vya NIDA, na kumuagiza Naibu Waziri wa Mambo ya ndani afike Kagera kuungana na Katibu Mkuu kuwa sehemu ya msafara wa ziara hiyo, ili atolee ufafanuzi na kujibu malalamiko ya wananchi kuhusu jambo hilo. @ccmtanzania @nchimbie

Maisha: Mdomo unapokiwakilisha kidole
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Agosti 10, 2024