Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imejipanga kujenga uchumi jumuishi unaowainua wananchi wote na kuwawezesha wananchi kunufaika ipasavyo kupitia uwekezaji unaofanywa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Dkt. Samia aliyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya Nanenane yaliyofanyika katika uwanja wa Nanenane Nzuguni.

Amesema Serikali imeongeza bajeti kwa ajili ya kilimo, mifugo na uvuvi ili uwekezaji huo ulete mageuzi makubwa kwa kuongeza maeneo ya umwagiliaji, matumizi ya mbolea, uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora, kuimarisha huduma za ugani, kuboresha miundombinu ya kuhudumia mifugo pamoja na upatikanaji wa huduma za ugani, chanjo, majosho na masoko.

Rais Dkt. Samia pia amesema serikali imeendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya mifugo, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya uvuvi, ukuzaji wa viumbe maji na utafutaji wa masoko na utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa wavuvi na wafugaji.

Vile vile, Rais Dkt. Samia amesema lengo la kujenga uchumi jumuishi, ni kuongeza tija katika sekta za uzalishaji na kupunguza umasikini wa kipato kwa mwananchi mmoja mmoja na kutumia sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kutengeneza ajira.

Aidha, Rais amesema jitihada hizi, pamoja na kusaidia Tanzania kuhakikisha upatikanaji wa chakula, pia zina mchango katika Pato la Taifa na uchumi kwa ujumla.

Amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuongeza bajeti katika utafiti ndio maana maabara na vituo vya utafiti vimezinduliwa ili kuwezesha nchi kufikia masoko ya kimataifa kupitia tafiti.

Dkt. Mwinyi: Bado tunahitaji Wawekezaji zaidi
Maisha: Mdomo unapokiwakilisha kidole