Matumizi ya simu za mkononi yanaweza kuathiri tabia ya Dereva, kutokana na maamuzi anayotaka kuyafanya barabarani, huku kukiwa na ushahidi kwamba dereva anayetumia simu wakati anaendesha chombo cha moto yupo katika hatari ya kupata ajali mara nne zaidi ya yule ambaye hatumiii simu.

Kitendo cha kupiga simu, huathiri uwezo wa dereva kuendelea kubaki barabarani inavyotakiwa na matokeo ya tafiti nyingi yanaonesha kwamba ufanisi wa dereva unapungua kwa kiasi kikubwa hasa katika kuendesha kwa spidi inayotakiwa, kufanya maamuzi na kuweka umbali kati ya gari lake na la mbele au la nyuma.

Kuna swali la kujiuliza, kuna sababu gani hasa ya kutumia simu wakati ukiendesha chombo cha Moto? Je facebook, meseji, Instagram, twitter, na whatsapp haziwezi kusubiri hadi usimame? Je meseji zinafutika? Ni afadhali kabisa mtu anayeongea kwenye simu huku anaendesha kuliko anayechat huku anaendesha.

 

Japo wote wapo kwenye hatari hiyo ya kupata ajali. Simu inaharibu umakini na uzingatiaji na inapunguza uoni, kwani macho mara nyingi yatakuwa kwenye simu na si barabarani, hivyo ni vema kupeana talaka na simu wakati wa kuendesha na njia sahihi ya kufanya hivi ni kuzima data na kuiweka simu mbali kabisa na usawa wa macho.

Simu hufanya usione alama za barabarani, taa nyekundu na kuna muda waweza jikuta ushavuka. Simu inafanya ubongo ulegeze mguu kwenye peda za breki au ukandamize zaidi, simu zinafanya tujisahau tukiwa kwenye usukani. Simu zinafanya tusione ishara za maelekezo kutoka kwa askari tukiwa kwenye foleni au kwenye mwendo.

Kwenye foleni Askari ameruhusu gari dereva bado uko busy na simu au askari amesimamisha magari wewe bado umezubaa na simu unajikuta unagonga au kuigusa gari ya mbele yako. Kisa, ni simu? Kwa mtu yeyote anayekupenda, inatakiwa ukishamwambia unaendesha tu, akate simu.

 

Asiyekupenda ataendelea kuchat na wewe au kusisitiza muendelee kuongea. Kama ni kwenye group, meseji utazikuta tu, wala haina haraka. Gari halitakiwi kuendeshwa huku ukiwa na msongo wa mawazo au akili haijatulia, hivyo simu inaweza kuchochea msongo wa mawazo hasa kutegemea na taarifa unayoipata kutoka kwenye simu.

Elimu kutoka kwa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani Nchini – RSA.

Zahoro: Yamalizeni mapema kabla ya uchaguzi
Dkt. Mwinyi: Bado tunahitaji Wawekezaji zaidi