Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imejipanga kuhakikisha vijana wanapata elimu bora inayohitajika katika soko la ajira.
Amewahakikishia vijana kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu ya ufundi, ujuzi, na maarifa kwa ajili ya kuwajengea vijana uwezo.
Dkt. Mwinyi aliyasema hayo wakati alipofungua Kongamano la Vijana la Kitaifa lililobeba kauli mbiu inayosoma “Kuwa Kijana wa Tofauti” katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Mbweni, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Aidha, amewataka vijana kuzichangamkia fursa zilizopo zinazoandaliwa na Serikali kwa lengo la kuzifikia ndoto zao.
Kuhusu suala la uongozi, ametoa wito kwa vijana kushiriki kikamilifu na kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025.
Wakati huo huo, katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi aliwatunuku vijana mbalimbali Tuzo za Umahiri kwa kufanya vizuri katika fani tofauti ambazo zimechangia kuwajengea uwezo vijana nchini.
Naye, mwanzilishi wa Taasisi ya Global Youth Empowerment, Amina Sanga, alimtunuku Rais Dk. Mwinyi Tuzo Maalum ya Uongozi uliotukuka katika jukwaa hilo.