Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema tayari Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 31.8 kupitia Wakala wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, ikiwemo kuwawezesha vijana. Tayari shilingi milioni 338.6 zimetolewa kwa makundi mbalimbali.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Vijana Kimataifa 2024, yaliyofanyika Golden Tulip Hotel, Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja na kueleza kuwa tayari vijana 500,000 wanaendelea kupata mafunzo ya stadi za maisha, mafunzo ya matumizi ya TEHAMA, na ujasiriamali.

Rais Mwinyi ameridhia maombi yaliyotolewa na vijana katika maadhimisho hayo, ikiwa ni pamoja na kuzingatia suala la maendeleo ya vijana katika mipango yao na kuongezwa kwa bajeti ya wizara katika masuala yanayohusu vijana na taasisi za mikopo ili kuwawezesha vijana kupata mikopo kwa wepesi na kwa urahisi.

Aidha, Dkt. Mwinyi amewataka vijana kushiriki kwa wingi na kugombea katika uchaguzi mkuu ujao na kuahidi kuongeza idadi ya vijana katika uteuzi wa nyadhifa mbalimbali Serikalini.

Naye, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, na Michezo, Tabia Maulid Mwita amesema juhudi zinaendelea za kuimarisha vituo vya stadi za maisha na tayari Serikali imetenga shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikubwa cha kuwawezesha vijana.

Simulizi: Amedhamiria, anataka kuvunja Kitanda
Ngeze: DED, Wenyeviti Halmashauri msivutane leteni maendeleo