Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika – CDC, kimetangaza hali ya dharura ya afya ya umma, kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Mpox unaokua kwa kasi, huku wakiitaka jamii kuweka jitihada ili kuzuia na kukomesha maradhi hayo.
Mwenyekiti wa CDC Africa, Jean Kasenya amesema hatua hiyo inafuatia kurekodiwa kwa visa 38,465 vya ugonjwa huo, ambao awali ulijulikana kama Homa ya nyani, katika nchi 16 Barani Afrika tangu Januari 2022, vifo 1,456 na ongezeko la asilikia 160 ya kesi kwa mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Amesema, “mlipuko wa Mpox sasa umevuka mipaka, na kuathiri maelfu ya watu katika bara letu, ninaamua kusema, kwa moyo mzito lakini kwa dhamira isiyotetereka kwa raia wetu, kwa raia wetu wa Kiafrika, kwamba tunatangaza mlipuko wa Mpox.”
Kuenea kwa aina hii mpya ya virusi, kunafuatia kugunduliwa kwa ugonjwa huo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC Septemba 2023 na kuitwa “Clade Ib” ikiwa ni hatari na inayoambukiza zaidi kuliko ile ya awali.