Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na Taasisi za Mabenki Yasiyo na Mipaka (Bankers without Boundaries) kuwekeza miradi ya kipaumbele na yenye tija kwa nchi.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 14, 2024, alipokutana na Mkuu wa Taasisi ya Mabenki Yasiyo na Mipaka ambayo Makao Makuu yake yapo nchini Uingereza, Matteo Scollabrino aliyefika Ikulu na ujumbe wake.
Amesema sekta ya Uchumi wa Buluu, Kilimo, Nishati, Miundombinu, na Afya ni sehemu ya miradi ya kipaumbele kwa Serikali na inahitaji msukumo wa ziada ili iweze kuleta tija kwa nchi.
Naye Mkuu wa Bankers Without Boundaries, Matteo Scollabrino, amesema taasisi hiyo ambayo imeingia nchi 40 duniani inalenga kushirikiana na Serikali kwa kuwekeza katika miradi isiyo na athari za kimazingira pamoja na kupunguza mzigo wa gharama za uendeshaji na tayari imetenga kiasi cha Dola Milioni 500 kwa kufanikisha azma hiyo.
Kikao hicho ambacho kimefanyika Ikulu Zanzibar kimehudhuriwa na watendaji wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango na Presidential Delivery Bureau (PDB).