Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, ametoa ufafanuzi kuhusu utaratibu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, Mchengerwa, amebainisha kuwa, kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, huku wagombea wakitakiwa kuwa na sifa ya uanachama na wadhaminiwa wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Mchengerwa amebainisha hayo leo Agosti 15, 2024, jijini Dodoma alipokuwa akitoa tangazo la uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.

Amesema, “Uchaguzi utaanza saa mbili kamili asubuhi hadi saa kumi kamili jioni, ninawatakia uchaguzi mwema, amani na utulivu katika kipindi chote kabla na baada ya uchaguzi.”

Aidha, amesema, kampeni za uchaguzi zitadumu kwa siku saba kabla ya siku ya uchaguzi, ambapo kila chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi kitawasilisha ratiba ya mikutano ya kampeni kwa msimamizi wa uchaguzi kabla ya siku saba za kuanza kampeni.

Chaguzi hizi zitahusisha kuwachagua wenyeviti wa vijiji, wajumbe wa Halmashauri ya vijiji, wenyeviti wa mitaa, wajumbe wa kamati za mitaa na wenyeviti wa vitongoji.

Baraza la Vyama vya Siasa lazifagilia 4R za Rais Samia
Wakutana kujadili mabadiliko mikataba ya uongozi EAPP