Kamati ya Kudumu ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -TAMISEMI ikiongozwa na Mweneyekiti Mhe. Justine Nyamoga leo imeielekeza Menejimenti ya Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo kuongeza mabweni katika chuo hicho ili kuwasaidia wanafunzi kwa kukaa katika maeneo salama na kuongeza mapato ya Chuo.
Nyamoga ameyasema hayo katika kikao cha majumuisho mara baadaa ya kukamilika kwa ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na chuo hizo ambayo ni ujenzi wa Madarasa, ujenzi wa Jengo la Utawala na ujenzi wa nyumba za wakufunzi.
“Maelekezo ya kamati ni kwamba ujenzi wa mabweni ni jambo mhimu mnaweza kukopa kutoka Bodi ya Mikopo ili kukamilisha ujenzi huo kwani mtakuwa na uwezo wa kurudisha kupita mabweni”
Amesema ujenzi wa mabweni ni jambo mhimu sana kwa maslahi mapana ya wanafunzi wa Chuo hicho.
Aidha kamati imefurahishwa na namna ambavyo Chuo hicho kimekuwa kikiendesha shughuli zake hasa katika kuzalisha Watumishi mbalimbali ambao wamekuwa wakitumika katika Serikali za Mitaa katika maeneo mengi Nchini.
Pia kamati imezielekeza Ofisi za Halmashauri kuwa na utaratibu wa kupeleka watumishi wao katika Chuo hicho cha Serikali za Mitaa kwa lengo la kuongeza ujuzi zaidi hasa katika kipindi ambacho Wanafunzi wa chuo hicho wanapokuwa likizo.
Akitoa neno la shukrani Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Adolf Nduguru ameishukuru Kamati kwa uamuzi wao wa kutembelea katika Chuo hicho na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliotolewa na Kamati kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma katika Chuo hicho.