Aliyekuwa Rais wa Ghana, Kwame Nkrumah alikuwa akielekea China wakati mapinduzi yaliyoungwa mkono na CIA yalipofanikiwa kumpindua.
Bila kuwa na taarifa hiyo, alilakiwa na Waziri Mkuu wa China wa kipindi hicho, Zhou Enlai kwenye Uwanja wa Ndege wa Beijing na baadaye Enlai alimpasha habari Nkrumah kuhusu kilichotokea na mwanzoni Nkurumah alijitahidi kuukubali ukweli lakini alielewa bada ya habari kuanza kuenea kwa kasi.
Ujumbe wa Nkrumah wa maofisa 90 ulisambaratika haraka hapo Nkrumah akakimbilia Guinea, ambapo Rais Sekou Toure alimpa hifadhi ya kisiasa na hata hivyo, baada ya kifo cha Nkrumah mwaka 1972, kulizuka mzozo kati ya Toure na kiongozi wa jeshi la Ghana, Kanali Ignatius Acheampong, kuhusu mahali pa kumzika Nkrumah.
Toure aliweka ngumu kuachia mwili wa Nkrumah ili kumpumzisha, kuachiliwa kwa washirika wake na kukaribishwa rasmi kwa mabaki yake nyumbani, alitaka pia kaburi la Nkrumah liwekwe mbele ya jengo la Bunge la Ghana na maafisa wake wa zamani kurejeshwa.
Viongozi wa Afrika wakiwemo Marais William Tolbert wa Liberia, Siaka Stevens wa Sierra Leone na Jenerali Yakubu Gowon wa Nigeria waliingilia kati kumshawishi Toure kuachilia mwili huo. Walisema kuwa ni muhimu kwa heshima na taswira ya Mwafrika nje ya nchi.
Hatimaye, Toure alikubali, na mwili wa Nkrumah ukarudishwa Ghana kwa mazishi.