Mwenyekiti wa Chama cha ACT –Wazalendo Taifa, Othman Masoud Masoud Othman, amesema kwamba vitisho kutoka kwa Kamshina wa Polisi Zanzibar Hamad Khamis, dhidi ya viongozi wa chama hicho yanamsukumo wa kisiasa kutoka kwa viongozi walioelemewa na hoja za chama hicho.
Mhe. Othman ameyasema hayo huko Ofisi Kuu ya chama hicho iliyopo Vuga mjini Unguja alipozungunza na vyombo vya habari kutoa ufafanuzi dhidi ya taarifa ya Kamshina wa Polisi Zanzibar aliyoiita ya vitisho kwa viongozi wa ACT Zanzibar ikidai kuwaonya viongozi wa kisiasa wanaotoa matamshi ya kuvuruga amani na kejeli dhidi ya utawala halali ambayo alisema iliwalenga wa chama hicho.
Amefahamisha kwamba Zanzibar yapo matukio kadhaa ya hivi karibuni ambayo polisi walipaswa kuchukua hatua za kisheria ikiwemo vitendo vya kikatili , kiharamia na uhalifu pamoja na uvunjifu wa amani ambayo jeshi hilo halikuweza kuchukua hatua yoyote dhidi ya wahusika licha ya kuwafahamu.
Amesema kwamba iwapo jeshi hilo lingekuwa na dhamira ya kweli ya kudhibiti uvunjifu wa amani na kwavile jinai haina ukomo, polisi walipaswa kuchuka hatua mapema ikiwemo kuchunguza kuuawa kwa watu 21 katika maeneo mbali mbali ya visiwa vya Unguja na Pemba katika miezi ya Oktoba na Novemba mwaka 2020 kwenye uchaguzi wa mwaka huo.
Amefahamisha kwamba licha ya kuyafahamu mauaji hayo, polisi wameshindwa hata kufungua jalada dhidi ya matendo hayo angalau kwa uchunguzi na kwamba polisi hawapaswi kufanya kazi kwa kuelemea upande mmoja wa siasa na kutoa vitisho visivyo vya msingi kwa upande wa pili.
Aidha amesema kwamba katika mfululizo wa matukio ya uvunjifu wa amani, watu 18 katika kipindi hicho walipigwa hadi kupata ulemavu na wa kudumu na wengine zaidi ya 700 kujeruhiwa baada ya kupigwa na wengine kubakwa na pia viongozi waandamizi wa ACT walitekwa na kupigwa na kuteswa huko Hanyegwa mchana na kwamba polisi hakufungua hata jalada la upelelezi dhidi ya matukio hayo na mengine kadhaa.
Sambamba na hayo pia kuna mama kikongwe mkaazi wa mtoni aliyepigwa bomu la machozi na polisi akiwa nyumbani kwake na kumjeruhi bila hatia na baadaye kumsababishia kifo, lakini polisi hawakuona kwamba huko ni kuvunja amani na hawakuchukua hatua yoyote.