Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wazazi kuhakikisha vijana wao wanakwenda shule za sekondari kwani bila elimu hawawezi kufika mbali.
Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mtondo kilichopo Kata ya Nambiranje, Ruangwa Mkoani Lindi.
Alisema Wilaya wilaya hiyo ina shule tatu za wasichana pekee ambazo ni Liuguru, Ruangwa Girls na Lucas Malia na kwamba Serikali imefanikiwa kujenga shule za sekondari za kidato cha tano na sita za Ruangwa, Mbekenyera, Nkowe, Lucas Malia na Hawa Mchopa huku Shule ya sita ya Mandawa ikitarajia kukamilika hivi karibuni.
Kwa upande wa sekta ya maji, Majaliwa alisema vijiji vyote 90 vya wilaya vilichimbiwa maji kupitia taasisi ya GAIN lakini kwa sasa hayatoshi. Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kuwajulisha kwamba Serikali imetoa sh. bilioni 49 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji kutoka Nyangao ambao utavinufaisha vijiji 34 vya wilaya ya Ruangwa na vijiji 29 vya wilaya ya Nachingwea.
Kuhusu umeme, alisema laini zimeshaenda kwenye kila kijiji na kwamba Serikali hivi sasa inashughulika kuweka umeme kwenye ngazi ya vitongoji na upande barabara, alisema kuna changamoto ya kufika kijiji cha Mtondo ambayo tayari iko kwenye mpango wa ujenzi.
Awali, Diwani wa Kata ya Nambiranje, Mossa Mohammed Mtejela alimuomba Waziri Mkuu awasaidie, ili waongezewe fedha za ujenzi wa barabara ya kutoka Mtondo hadi Mkaranga Sekondari yenye urefu wa kilometa saba.