Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza kurejeshwa kwa huduma za kijamii za elimu na afya katika Tarafa ya Ngorongoro.
Lukuvi ameyasema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa kata 11 zilizopo Tarafa ya Ngorongoro waliokesha kwa siku 5 wakitaka kujua hatima ya malalamiko yao.
Amesema, “kila Diwani aende kwenye Kata yake afafanue huu ujumbe wa Rais Samia, Wananchi hawa waelezwe kwamba hamna aliyezuiwa kupiga kura, Rais ameelekeza wapige kura kama Wananchi wengine.”
“Mabango haya yana ujumbe mwingi sana, Rais amenituma niseme ataandaa siku na mahali ambapo atakutana na Wawakilishi wa Jamii ya Ngorongoro, ili mkamwambie Rais moja kwa moja, RC Makonda hakikisha unasimamia uamuzi wa Rais na kwamba vijiji vilivyopo vinabaki vilevile,” alisema Lukuvi.
Aidha, Lukuvi pia amemuambia Mkurugenzi wa Ngorongoro kuwa huduma zimekuwa hazitolewi vizuri, na kumuagiza zote zilizokuwa zimesitishwa zitolewe kikamilifu.